Jumatano , 7th Dec , 2022

Klabu ya soka ya Geita Gold umefikia maridhiano ya kusitisha mkataba na aliyekuwa mchezaji wao George Enock Mpole kuanzia leo Disemba 7 ,2022.

Kupitia barua iliyovuja ya mshambuliaji huyo kusitishiwa mkataba ilisema,

 "Uongozi wa klabu ya Geita Gold, unakutaarifu rasmi ya kwamba mkataba wako wa ajira kati ya klabu na wewe (Mpole) umemalizika rasmi leo baada ya pande mbili kukubaliana na uko huru kujiunga na klabu yoyote kuanzia leo,"

"Tunachukua fursa hii pia kukushukuru kwa kazi, ushirikiano na utendaji mzuri uliouonyesha kwa klabu kwa kipindi chote tangu tumekuwa pamoja mpaka tulipokubaliana kusitisha mkataba wetu. Pia tunakutakia kila la kheri katika maisha yako ya mpira wa miguu," imesema taarifa hiyo.

Sakata la George Mpole na klabu yake limeanza kufukuta tangu Oktoba 13, mwaka huu baada ya mchezo wa raundi ya saba ambapo nyota huyo hakuungana na wenzake kwa maandalizi ya michezo iliyofuata.

Mpole hakuonekana kambini kwenye michezo mbalimbali ya timu hiyo kwa kile alichoeleza kuumwa na yuko nyumbani kwao mkoani Mbeya anatibiwa kwakuwa madaktari wa timu hiyo wameshindwa kumpa tiba huku baadhi ya taarifa zikidai mshambuliaji huyo anadai stahiki zake za mshahara wa mwezi wa 10.