Jumapili , 11th Feb , 2024

Klabu ya Young Africans kupitia kwa Rais wake Eng. Hersi Said leo wametangaza kuwa mdhamini na mfadhili wa klabu hiyo Gharib Said Mohamed kupitia makampuni yake ya GSM atajitolea kushiriki kwenye ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Injinia  Hersi ameweka wazi kuwa klabu hiyo itaanza ujenzi wa uwanja wao kwenye eneo la Jangwani ambali lipo karibu na makao makuu ya klabu hiyo.

“Baada ya mazungumzo ya muda mrefu na mfadhili na mdhamini wa klabu yetu, Gharib Said Mohamed , nipende kuwataarifa wanachama na mashabiki wa klabu yetu kuwa leo GSM ameridhia kwa dhati kushiriki kwenye kufanikisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Yanga katika eneo la makao makuu ya klabu yetu Jangwani, Jijini Dar es salaam,” amesema  Hersi.

 

Ni klabu tatu pekee nchini zenye viwanja vyake na klabu mbili ndizo zenye viwanja vinavyokidhi ubora wa kuchezea Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.

Klabu hizo ni JKT Tanzania , Singida Fountain Gate na Azam fc . Ni Azam na JKT Tanzania pekee ndio zenye uwanja unaotumika kwa michezo ya Ligi kuu.