Jumanne , 31st Jan , 2023

Uongozi wa klabu ya Singida Big Stars umejinasibu kupata ushindi na kuondoka na alama 3 mbele ya kikosi cha Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu NBC Tanzania unaotaraji kuchezwa Ijumaa Februari 3, 2023 kwa wanajivunia sajili za wachezaji wapya walizozifanya.

Wachezaji wa Singida Big Stars

Akiongea kwa niaba ya Uongozi wa Singida Big Stars, Afisa Habari wa klabu hiyo, Hussein Massaza ameiambia EATV kuwa, maingizo mapya yamewafanya imara zaidi hivyo wamejipanga kuondoka na alama 3.

''Hii haitakuwa mechi nyepesi. Itakuwa ni kama vita na kama nilivyosema kwamba kila mchezo una mipango yake na muda ukifika tutajipanga kwa mechi hiyo. Kwani lengo letu ni kuhakikisha tunashinda kushinda kila mchezo kwa kuwa huku hakutafutwi alama bali ushindi,” Amesema Massaza

Kwa upande wa wachezaji, kiungo wa timu hiyo, Kelvin Nashon amesema wachezaji wote wapo salama na wana morali kubwa ya kutaka kucheza mchezo huo na kuibuka na ushindi mbele ya mnyama Simba SC.

Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa duru la kwanza Ligi Kuu NBC Tanzania Novemba 9, 2022 ambapo walitoka sare 1-1. Singida Big Stars ipo nafasi ya 4 na alama 43 ilhali Simba SC ipo nafasi ya 2 ikiwa na alama 50 na kinara Yanga alama 56.