Alhamisi , 18th Feb , 2016

Mashindano ya riadha ya Kilimanjaro Marathon yatakayofanyika Februari 28 mwaka huu, yatatumika kupata wachezaji wenye viwango vya kushiriki Olympic mjini Rio, Brazil baadaye mwaka huu.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Riadha Tanzania RT Ombeni Zavara, amesema mashindano ya Kilimanjaro Marathon, sehemu ya kupata pointi kwa wanariadha na atakayeshindwa kwenye mbio hizo atarejeshwa kwao.

Kwa mujibu wa viwango vya dunia atakaye fuzu ni yule atakayekimbia muda si chini ya muda wa masaa 2 na dakika 19.

Zavara aliyekuwa Kilimanjaro kwenye kambi ya timu ya taifa ya riadha, iliyopo chuo cha misitu mjini Moshi, amesema mwisho wa kufuzu kwa Olympic ni Mei 30 mwaka huu na baada ya hapo hakuna atakaye ruhusiwa kupeleka mchezaji Rio.

Hadi sasa Tanzania ina wachezaji wawili tu waliofuzu ambao ni Felix Alphonce na Saidi Juma na wengine wataendelea kufanyiwa mchujo kwenye mashindano mbalimbali kabla ya Mei 30.