Jumatano , 1st Jun , 2016

Asilimia 70 ya watanzania hawana uelewa kuusiana na kupata msaada wa kisheria, uwepo wa wasaidizi wa kisheria na jinsi gani wanaweza kusaidiwa katika matatizo ya kisheria.

Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Msaada wa Sheria (LSF), Bi. Scholastica Jullu, amesema hivi sasa wasaidizi wa sheria 4,000 wapo nchi nzima katika ngazi ya wilaya kuwasaidia watanzania katika utatuzi wa migogoro ya kisheria.

Scholastica amesema huduma za kisheria zina gharama kubwa na wakati mwingine hupelekea msongamano wa kesi katika mahakama za mwanzo hivyo wasaidizi hao watahakikisha kesi zote zisizo za kijinai zinatatuliwa.

Kwa upande mwingine Bi. Scholastica amesema ni vyema serikali ikaunda sheria ya msaada wa kisheria sambamba na kuwathamini wanaotoa msaada wa kisheria kote nchini kwani uwepo wao ni muhimu kwa kusimamia haki za watanzania mbalimbali wasio jua haki zao na mahala pa kwenda kutafuta haki.