Mkurugenzi wa Usajili na Ithibati wa NACTE, Bi Twilumba Mponzi
Ofisi hizo zitawekwa hasa maeneo ya vijijini ambayo yamekuwa na changamoto kubwa ya kuwepo kwa vyuo vingi ambavyo havijasajiliwa na Baraza la Taifa la Elimuya Ufundi NACTE na kusababisha hasara kwa wazazi na wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo.
Akizungumza na East Africa TV, Mkurugenzi wa Usajili na Ithibati wa NACTE, Bi Twilumba Mponzi amesema hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali itasaidia baraza hilo kupunguza vitendo vya utapeli wa fedha kwa wanafunzi na wazazi ambao hawana uelewa wa taratibu za kugundua vyuo vyenye vibali vya serikali.
Amesema baada ya kuanzishwa kwa ofisi hizo za kanda wamegundua vyuo vingi ambavyo havina sifa za kuwa vyuo, vimesajili wanafunzi na kuanza masomo yao kinyume cha sheria, hivyo baraza hilo tayari limeanza kuvifungia na kuchukua hatua stahiki za kisheria sambamba na kuhakikisha wanafunzi wanaokumbwa na tatizo hilo wanapata stahiki zao.
Aidha ameongeza kuwa sambamba na kuhakiki vyuo hivyo pia wanakagua sifa za wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo hivyo kwa kuwa wengi wao hawana sifa zilizowekwa na NACTE.
Amesema wazazi na wanafunzi wanaojiunga na vyuo wahakikishe wanaenda NACTE kuhakikisha kama vyuo hivyo ambavyo wanataka kujiunga vimesajiliwa na wizara hiyo ili kuepusha mgororo ambao unaweza kutokea siku za mbeleni.
Amesema mkoa wa Dar es salaam unaongoza kwa kuwa na vyuo ambavyo havijasajiliwa na NACTE.