Alhamisi , 13th Oct , 2016

Serikali imeombwa kuwaangalia wanawake wajasiriamali kama kundi linalopaswa kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa sera ya ujenzi wa viwanda

Muelimishaji Mkuu Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato nchini TRA Bi. Rose Mahendeka

Hiyo ni kutokana na utayari uliooneshwa na wanawake hao ambao wengi wao ndiyo wamiliki wa biashara zenye mwelekeo wa ujenzi wa viwanda vidogo vidogo.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Wajasiriamali ya (TWCC) Bi. Fatma Kange, wakati wa mafunzo kuhusu elimu ya kodi, usajili wa makampuni na mbinu za kibiashara, mafunzo yaliyoandaliwa kwa wanachama na wasio wanachama wa taasisi hiyo kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya wafadhili na watoa mada katika mafunzo hayo ni Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ambapo Muelimishaji Mkuu Mwandamizi Bi. Rose Mahendeka anaeleza kusudio la kufadhili mafunzo hayo kuwa ni kujaribu kuyafikia makundi muhimu katika uchumi wakiwemo wanawake wajasiriamali ambao biashara zao zimekuwa na mchango kwa uchumi wa nchi lakini wamekuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kodi.

Kutokana na mwitikio mkubwa, Mwenyekiti Mwanzilishi wa Taasisi hiyo Bi. Dina Paulina Bina amesema hiyo ni ishara kuwa wanawake nchini wameamka kuchukua nafasi zao katika uchumi na kwamba kuna haja ya serikali kuelekeza nguvu kubwa katika kuwapa wanawake fursa ya kustawi kiuchumi.

Mwenyekiti wa sasa wa Taasisi hiyo Bi. Jacqueline Maleko yeye amesema wanajisikia faraja kuwa bega kwa bega na Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuwainua wanawake kiuchumi na hasa kipindi hiki baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kumteua Makamu huyo wa Rais wa Tanzania kuwa mmoja wa wajumbe wa Jopo la Hali ya Juu la Umoja wa Mataifa linaloangalia shughuli za uratibu wa kuwainua wanawake kiuchumi.