Jumatatu , 15th Jan , 2018

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Ndugu Wallace Karia amempongeza mwanamichezo na mwanasheria msomi Dr.Damas Ndumbaro kwa kushinda kiti cha Ubunge Jimbo la Songea Mjini.

Rais Karia ametoa pongezi hizo leo na kueleza kuwa  ushindi wa Dr.Ndumbaro unaongeza idadi ya wanamichezo ndani ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanaweza kuwa chachu ya maendeleo ya michezo hususani mpira wa miguu.

“Tunaamini uwezo wa Dr.Ndumbaro katika uongozi tumemuona katika mpira wa miguu akiongoza katika sehemu mbalimbali hakika uwezo wake wa uongozi ni mkubwa na atasaidia sana kukua kwa sekta hii ya michezo'', amesema Karia.

Dr.Ndumbaro amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye mpira wa miguu na hivi karibuni Rais Karia alimteuwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya rufaa ya leseni za klabu.

Dr.Ndumbaro aligombea katika Jimbo la Songea Mjini   kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda kwa kura 45762 akiwazidi wagombea wengine 7 kutoka vyama mbalimbali.