Jumapili , 20th Mei , 2018

Wawakilishi wa Kimataifa wa Tanzania klabu ya soka ya Yanga, imejikuta ikipitia nyakati ngumu uwanjani na nje ya uwanja kiasi cha nahodha Nadir Haroub, kukiri kuwa hakuna kipindi kigumu wachezaji wanapitia ndani ya klabu hiyo kama hiki.

Yanga ambayo ilianza vizuri msimu kwasasa imepoteza mwelekeo na hata matumaini ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi japokuwa ina mechi mbili nyuma ya Azam FC ambao wapo katika nafasi hiyo.

Tangu aondoke kocha George Lwandamina Yanga haijaonja ladha ya ushindi kwenye mechi 9 mfululizo si kwa michezo ya Ligi ya nyumbani bali hata kimataifa ambako inacheza hatua ya makundi ya Kombe la shirikisho.

Zifuatazo ni mechi 9 ambazo zimeweka rekodi na historia kwa klabu hiyo kukosa ushindi kwenye mecxhi nyingi mfululizo jambo ambalo miaka ya hivi karibuni halikuwepo.

April 11, 2018 Yanga ilitoka sare ya 1-1 na  Singida United, April 18, 2018, Yanga ikafungwa 1-0 na Walaita Dicha ugenini. April 22, 2018 ikatoka sare ya 1-1 na Mbeya City. April 29, 2018, Yanga ikafungwa 1-0 na Simba kabla ya Mei 6 kufungwa 4-0 na USM Alger.

Mei 10, 2018 Yanga ilifungwa 2-0 na Prison huku Mei 13 ikakubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar. Mei 16, Yanga ikatoka sare ya 0-0 na Rayon Sports. Jana Mei 19 ikakubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mwadui FC na kukamilisha mechi 10 bila ushindi.