Jumatatu , 13th Aug , 2018

Uongozi wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ umesema kuwa malengo yao msimu huu katika Ligi Kuu Bara ni kushinda kila mechi watakayoteremka uwanjani iwe nyumbani au ugenini na hakuna wa kuwazuia kwani wana wachezaji wenye uwezo wa kufanya hivyo.

Mshambuliaji wa Coastal Union, Ali Kiba.

Coastal ambao hivi karibuni wamemsajili mwanamuziki Alikiba, kwa sasa wanaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Saruji yanayosimamiwa na makocha, Juma Mgunda, Joseph Lazaro pamoja Salim Waziri (Tupa).

Akizungumza na wanahabari, makamu mwenyeketi wa kamati ya usajili, Abdallah Mohamed amesema usajili waliofanya kwa wachezaji wazoefu na chipukizi ndiyo sababu kubwa ya kuamini watafanya vizuri msimu huu.

Malengo yetu kwanza ni kuhakikisha tunashinda michezo hii mitatu ya nyumbani dhidi ya Lipuli FC, Biashara United na KMC baada ya kuzipata hizo ndiyo itatuongezea hamasa ya kwenda kufanya vizuri katika mechi za ugenini zinazofuata,” amesema Abdallah.

Kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda amesema wachezaji wote wapo fiti na wanaendelea na mazoezi vizuri, wapo tayari kwa mapambano yoyote na kusisitiza kuwa muhimu ni wadau wa michezo mkoani humo kuendelea kuwaunga mkono.