Jumatatu , 1st Oct , 2018

Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu, amesema  pamoja na uvumi unaoendelea kuwa klabu yake ina mpango wa kumsajili kiungo Paul Pogba wa Manchester United, lakini jambo hilo ni gumu.

Kushoto ni Paul Pogba na Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu.

Bartomeu amevunja ukimya huo na kuliambia gazeti la 'The Times', kuwa mara nyingi mawakala wamekuwa wakitangaza wachezaji wao kuwa wako sokoni lakini wanapowasiliana na viongozi wa klabu wanakanusha.

''Sio Pogba tu, ni wachezaji wengi unaweza ukasikia wapo sokoni na wengine unakuwa unawahitaji lakini ukimpigia simu bosi wa timu anasema hauzwi na wanataka kubaki naye'', amesema.

Alipoulizwa endapo ana mpango wa kutuma ofa kwa Man United mwezi Janauri, Bartomeu alisema jambo hilo si kwa Pogba pekee bali kwa nyota wengi wanaowahitaji lakini changamoto ni kuwa timu zao hazitaki kuwauza.

Siku za hivi karibuni imeonekana kutokuwepo kwa mahusiano mazuri, kati ya kocha Jose Mourinho na Pogba lakini jumamosi iliyopita, nyota huyo alianza kwenye mchezo dhidi ya West Ham United ambapo Man United walipoteza kwa mabao 3-1.