
Akizungumza na umati wa watu waliojitokeza kwenye hafla hiyo Rais Magufuli amesema,"hivi punde tumeelezwa tangu mfumo huu ufanye kazi, umeleta faida, umeweza kutambua idadi ya watumiaji simu na internet, na serikali imepata bilioni 93.65, bila mfumo huu hizi bilioni zingekuwa kwenye mifuko ya watu".
Miongoni mwa majukumu ya mfumo huo mpya ni kupata takwimu za mawasiliano ya simu za ndani na nje ya nchi, ambazo zimekuwa zikiratibiwa na makampuni ya simu Tanzania, kuhakiki takwimu za mapato ya watoa huduma wa ndani, kupata takwimu za sauti, matumizi ya data na jumbe fupi, kujua simu za ulaghai, kutambua takwimu za gharama za ada fedha mtandaoni, kutambua taarifa za line za simu, kufungia simu zenye namba feki.
Akizungumza mbele ya hafla hiyo, Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba amesema, "watoa huduma walikuwa wanalipwa fedha kidogo na kampuni za nje za simu zilipokuwa zikiingia Tanzania lakini kwa mfumo huu wa TTMS kiwango cha fedha za kulipwa sasa kimeongezeka".