Jumatatu , 3rd Jun , 2019

Mama aliyejifungua watoto mapacha wanne, Radhia Solomon (24) mkazi wa Chemchemi  Magomeni  jijini Dar es salaam na kutelekezwa na mmewe kwa madai ya kukwepa majukumu amewasili bungeni na kuahidiwa kupatiwa msaada.

Radhia akiwa na watoto wake pamoja na baadhi ya wabunge.

Leo Juni 3,2019, Radhia amewasili bungeni jijini Dodoma ambapo bunge limeridhia kila mbunge wa kiume kumchangia shilingi laki moja na  kila mbunge wa kike kumchangia shilingi elfu hamsini fedha ambazo zitatumika kumsaidia kujikimu na kuwatunza watoto hao.
 
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma, Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema  jukumu la utunzaji wa watoto ni la kila jamii, hivyo bunge limeamua kufanya mchango huo kwa wabunge ili kumsaidia mama na watoto huku akiwaasa wanaume kuacha tabia ya kutelekeza familia zao.
 
Radhia Solomon alijifungua watoto mapacha wanne Januari 8, 2019 katika  hospitali ya Muhimbili Dar es salaam, watoto wa kike wawili Faudhia  na Fardhia  pamoja na wa kiume wawili Suleiman na Aiman  ni pacha wanne ambao  kila mmoja alikuwa na mfuko wake wa uzazi  na gharama ya kuwanunulia maziwa ya kopo  ni shilingi elfu 40 kwa siku  kwani  alipojifungua afya yake haikuwa nzuri kunyonyesha hali iliyosababisha mumewe kushindwa kumudu gharama na kuwatelekeza