Jumatatu , 3rd Feb , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ameeleza ni kwa namna gani ndoa ya aliyekuwa Kamishna wa Ardhi Mary Makondo, ilivyotaka kuingia mashakani kutokana na watu wengi kumchukia, sababu ya misimamo yake aliyokuwa nayo.

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, kulia ni Mary Makondo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi.

Rais Magufuli ameyabinisha hayo leo Februari 3, 2020, wakati akieleza ni kwa namna gani anawafahamu viongozi walioapishwa leo Ikulu ya Jijini Dar Es Salaam, ambapo Mary Makondo, yeye ameapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kusema kuwa ataenda kuinyosha vizuri wizara hiyo kwa kuwa ina madudu mengi.

"Hawakumpenda sana kwa sababu ya misimamo yake na kwasababu hiyo nikasema huyu ambaye hawampendi ndiye atabaki palepale ili wale ambao hawampendi waumie vizuri sana, wamejitahidi pia kumuandikia vimeseji vya kumchafua na walitaka kumchonganisha na mume wake, nampongeza mume wake aliendelea kusimama imara" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amewapongeza wale wote walioapishwa na kuwataka wakafanye kazi kwa weledi huku wakisimamia maslahi ya nchi na Taifa kwa ujumla.