Jumatatu , 16th Nov , 2020

Kocha mkuu wa klabu ya Namungo ya Lindi, Hitimana Thiery amesema mchezo wao ujao ligi kuu dhidi ya Yanga utakuwa ni kipimo sahihi kwa maandalizi kabla ya kuikabili Al Rabita ya Sudan katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha wa Namungo, Hitimana Thiery(Pichani) akiwa katika majukumu ya klabu yake.

Akizungumza na East Africa Radio, Hitimana amesema licha ya kwamba ligi kuu na michuano ya kombe la shirikisho ni tofati, lakini itawajengea taswira ya namna walivyojiandaa katika maeneo tofauti tofauti.

''Mechi ya Novemba 22 dhidi ya Yanga ni kipimo kizuri kwetu, ninaiandaa timu kwa ajili ya mchezo huo lakini pia itakuwa inatupa taswira ya kikosi changu kabla ya kucheza na Al Rabita. Bado sijapata nafasi ya kuwajua wapinzani wetu kimataifa kwakuwa kuna ugumu wa kupata taarifa zao, lakini tutajiandaa kadri inavyowezekana.'' alisema Hitimana Thiery.

Katika hatua nyingine kocha huyo amesema amefarijika kurejea kwa wachezaji wake wengine waliokuwa majeruhi wakiwemo Jaffari Mohamed na Stephen Seyi pia Adam Salamba ambao wanaongeza upana wa machaguo katika kikosi chake.

Namungo itaiwakilisha Tanzania bara katika michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza katika nafasi nzuri VPL na kombe la FA.