Jumatano , 18th Nov , 2020

Kaimu msajili wa bodi ya nyama, Imani Sichwale, amesema Bodi ya Nyama  imejipanga kuandaa utaratibu  wa usajili wa wabeba nyama kwa njia ya pikipiki au bodaboda kutoka katika machinjio hadi kwenye mabucha mbalimbali ya nyama nchini.

Kaimu msajili wa bodi ya nyama, Imani Sichwale

Akizungumza na viongozi wa Umoja wa Wasafirishaji wa nyama kwa kutumia pikipiki wanaofanya shughuli zao kwenye machinjio ya Vingunguti, jijini Dar-es-Salaam, Sichwale amesema kuwa usajili huo utawawezesha kutambulika na kupewa utaratibu mzuri,wa kubeba nyama kwasababu nyama ni kitoweo muhimu sana kwa binadamu

Kwa mujibu wa taratibu na sheria hairuhusiwi kufanya biashara ya nyama kama haujasajiliwa na bodi ya nyama, na katika usajili huo bodi ya nyama imekuwa ikisajili magari ya kubebea nyama ila wabebaji wa nyama kwa njia ya pikipiki ndio waliokuwa hawajasajiliwa licha ya kuonekana wakisafirisha nyama.

Aidha Sichwale ameainisha kuwa kwa mujibu wa kanuni zilizopo za usajili na ukaguzi zinayohusu biashara ya nyama hairuhusiwi kusafirisha nyama kwa njia ya bodaboda,kwa muktadha huo bodi ya nyama ikaona ni vyema kuja na mpango wa kuwasajili ili waweze kutambulika huku akisema uwepo wa kanuni mbalimbali, miongozo na sheria ni kwa lengo la kuongeza ubora na usalama wa nyama nchini.