Jumatatu , 23rd Nov , 2020

Upande wa Utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa zamani wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor, uliowakilishwa na wakili Eliya Mwingira, umesema walitarajia upande wa Jamhuri ueleze umefika wapi

Mkurugenzi wa zamani wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor

Wakili Mwingira, ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon, kudai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika ambapo pia amedai kuwa wametimiza taratibu za makubaliano ya mshitakiwa huyo kukiri kosa''Plea Bagaining'' lakini  mpaka sasa hajapata ushirikiano wowote.

Aidha Hakimu Matembele amesema suala la ''Plea bagaining'' ni kati ya waendesha mashtaka na upande wa mshtakiwa hivyo Mahakama itahusika kusajili tu na si vinginevyo na hivyo kumtaka Wakili huyo kutokukata tamaa na kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 7,mwaka huu.

Kwa mujibu ya hati ya mashitaka inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari  mwaka 2013 na Mei mwaka juzi , mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya Agosti 13,  mwaka 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo huku akijua kuwa sio kweli.

Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Januari mwaka  2013 na Mei mwaka jana huko maeneo ya Upanga, mshitakiwa alijipatia sh.1,477,243,000 wakati akijua kuwa fedha hizo ni haramu na ni zao la kosa tangulizi la kughushi.