Alhamisi , 29th Apr , 2021

Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga linawashikilia watuhumiwa 231 kwa tuhuma za kupiga ramli chonganishi na kuwa chanzo cha mauaji ya imani za kishirikina, na kujihusisha  na unyang'anyi wa kutumia silaha na kukata mapanga.

Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Debora Magiligimba.

Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Debora Magiligimba, amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni maalum ya kukabiliana na kuzuia makosa mbalimbali ya uhalifu, ambapo amesema kati ya watuhumiwa hao 71 ni wanawake na 160 wanaume.

Amesema pia wamekamata bunduki 14, bangi kilogramu 65, mashamba ya bangi ekari sita, madawa ya kulevya aina ya heroine gramu 300, mirungi kilogramu tatu na gramu 250 pamoja na vitu mbalimbali zikiwemo boksi 30 za kondom zilizopigwa marufuku .

Kamanda Magiligimba amesema Mkoa wa Shinyanga waganga wengi wa jadi ni wanawake ambapo baadhi yao wamekamatwa kwa tuhuma za kupiga ramli chonganishi, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za matukio ili kuchukuwa hatua kabla ya kufanyika.