Jumanne , 28th Sep , 2021

Mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara kati ya klabu ya Polisi Tanzania na KMC uliopangwa uchezwe kwenye uwanja wa Ushirika moshi mjini mkoani Kilimanjaro sasa utachezwa kwenye dimba la Karatu kesho Septemba 29, 2021.

Wachezaji wa KMC wakishangalia moja ya bao kwenye msimu uliopita wa ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo ulibadilishiwa uwanja kutoka Ushirika na kupelekwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha lakini usiku wa jana Septemba 27, 2021 bodi ya Ligi iliwatarifu KMC kwa barua pepe kuwa watacheza Karatu.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa wawili hao kwenye mzunguko wa kwanza wa msimu mpya wa Ligi kuu Bara huku Afisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amejinasibu kuwa walikuwa na maandalizi bora ya msimu na kuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye msimu huu.

Christina amesema, “Tangu tulipoanza maandalizi kwa wachezaji wetu, kikosi kimefanya mazoezi ya kutosha na hasa ukizingatia kwamba tunakwenda kuanza ligi ambayo kimsingi inaushindani mkubwa, lakini kwa ujumla tumejiandaa kukabiliana na ushindani huo na matarajio yetu ni kuhakikisha tunakwenda kufanya vizuri katika michezo yetu”.