
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais Samia ametoa kauli hiyo akiwa Chato wakati akielekea katika ziara mkoani Kagera ambapo amesema serikali itaendelea kutoa ruzuku ili kuhakikisha bei zinashuka hadi pale dunia itakapokuwa sawa.
"Tunajaribu kutoa ruzuku na mwezi uliopita nilisema natoa ruzuku ya bilioni 100 kufidia kwenye mafuta ili bei zishuke, na mwezi huu bei zimeanza kushuka polepole, tutaendelea kutoa hiyo ruzuku mpaka duniani kukae sawa"
Aidha Rais Samia amesema madhara ya kupanda kwa bei ya vitu sio janga la Tanzania bali ni la dunia nzima huku akitolea mfano vita ya Urusi na Ukraine inavyoathiri zao la ngano.
"Moja katika nchi zinazopigana tulikuwa tunaagiza ngano kutoka kwao, karibu asilimia 45 au 50 tulikuwa tunategemea ngano kutoka huko, sasa haiwezekani, sisi kwetu ni afadhali ila kuna nchi nyingine mikate sasa ni kwa mgao"
Pamoja na hayo Rais Samia ameahidi kuendeleza miradi mbalimbali iliyoanzishwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati John Magifuli huku akikisisitiza kuwa alijifunza mambo mengi kutoka katika uongozi wake
"Awamu iliyopita nilikuwa Makamu wa Rais chini ya kaka yangu Marehemu John Magufuli, alinifundisha mambo mengi sana, nilisoma dhamira yake vizuri sana, niwahakikishie dhamira ile ile tutakwenda nayo, hakuna mradi ambao tuliuanza ambao utakufa, kwahiyo niwahakikishie halijaharibika jambo"