Jumapili , 18th Sep , 2022

Wananchi wa Kata ya Pwaga,  jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma, wanatarajia kuanza kunufaika na mradi mpya wa maji baada ya serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa maji kupitia Mkandarasi Pioneer Building Limited.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, George Simbachawene,

Hayo yamefanyika wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, George Simbachawene, alipokabidhi nakala ya mkataba wa ujenzi wa mradi huo maji kwa Diwani wa Kata ya Pwaga, Wilfred Mgonela katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Pwaga jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Mpwapwa.

"Nimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ametupatia fedha nyingi kiasi cha billioni 4.3, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Kata ya Pwaga utakaosaidia vijijji vitano vya, Maswala, Itende, Ng’onje, Mungui na Pwaga, lazima tuhakikishe tunasimamia vizuri mradi wa maji na kwa uwazi ili  wote tuwe na uwezo wa kuona kilichopo na kuondoa mianya ya vitendo vya udanganyifu katika utekelezaji wake," amesema Waziri Simbachawene

Aidha Waziri Ametoa wito kwa Mkandarasi Pioneer Building Limited kutekeleza mradi wa maji kwa kasi ili watu waanze kupata huduma ya maji, "Mradi huu utatoa ajira nyingi kwa wananchi ambazo zitasaidia kujenga uchumi wa kata ya Pwaga,".