Jumapili , 18th Sep , 2022

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuandika historia ya kufikisha umeme wa gridi mkoani Kigoma kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.

Mariam Ditopile, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Dodoma

Akizungumzia mafanikio hayo katika sekta ya nishati nchini, Mariam ambaye ni Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini amesema kutokana na hatua hiyo serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) inakwenda kuokoa mabilioni ya fedha kwa kuzima majenereta yaliyokuwa yakitumia fedha nyingi kuzalisha umeme katika maeneo ambayo yamefikiwa na umeme wa gridi. 

"Umeme wa Grid ya Taifa kufika Kigoma ina maana Shirika la Tanesco linaenda kuokoa kiasi cha sh. bilioni 22. 4 kwa mwaka. Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetengeneza historia ya kipekee kwenye sekta ya nishati. Nampongeza sana Rais Samia na Serikali ya Awamu ya Sita ameandika historia, umeme wa Grid ya Taifa umefika Kigoma na kwa mara ya kwanza umeme umefika Kakonko na Kibondo haikuwa Rahisi," amesema.

Mariam amesema jana TANESCO imefanikiwa kuzima majenereta ya Kibondo, Ngara na Biharamulo na kuanza rasmi kutumia umeme wa Grid ya Taifa jambo ambalo halijawahi kutokea tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.