Jumatano , 1st Oct , 2025

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila amehukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani kwa uhalifu wa kivita na uhaini.

Mashtaka hayo yanamshutumu Kabila kuunga mkono kundi la M23, kundi la waasi ambalo limesababisha uharibifu katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Kabila alitiwa hatiani siku ya Ijumaa na mahakama ya kijeshi kwa uhaini, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.

Alikana mashtaka, lakini hakufika mahakamani kujitetea. Pia aliikataa kesi hiyo na kusema mahakama inatumiwa kama "chombo cha ukandamizaji". Kwa sasa hajulikani alipo.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 54 aliiongoza DR Congo kwa miaka 18, baada ya kumrithi babake Laurent, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka 2001.

Kabila alikabidhi madaraka kwa Rais Félix Tshisekedi mwaka 2019, lakini baadaye walitofautiana na akaenda uhamishoni mwaka 2023.

Mwezi Aprili mwaka huu, rais huyo wa zamani alisema anataka kusaidia kutafuta suluhu ya mgogoro katika eneo la mashariki na aliwasili katika mji unaoshikiliwa na M23 wa Goma mwezi uliofuata.
Rais Tshisekedi alimshutumu Kabila kwa nyuma ya M23 na maseneta walimwondolea kinga yake ya kisheria, na hilo kufungua njia ya kufunguliwa mashitaka.

Mapema mwaka huu M23 ilitwaa udhibiti wa maeneo makubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini, ikiwa ni pamoja na Goma, jiji la Bukavu na viwanja viwili vya ndege.

Umoja wa Mataifa na nchi kadhaa za Magharibi zimeishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono M23, na kutuma maelfu ya wanajeshi wake nchini DR Congo.

Lakini Kigali inakanusha mashtaka hayo.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya waasi na serikali yalifanyika mwezi Julai, lakini umwagaji damu umeendelea.