
Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, ambaye amefariki dunia jana Jumatano kutokana na mshtuko wa moyo, akiwa Koothattukulam katika wilaya ya Ernakulam, Kerala kwa matibabu nchini India utazikwa siku ya Jumapili, Oktoba 19, 2025 nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya.
Tangazo hilo limetolewa na Naibu Rais Kithure Kindiki, mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, pamoja na kaka mkubwa wa Odinga, Dk Oburu Oginga baada ya familia kuomba mazishi yafanyike haraka ndani ya saa 72 baada ya kifo kama alivyoomba Odinga enzi za uhai wake.
Mwili huo unatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Jomo Kenyatta nchini Kenya leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 majira ya 8:30 asubuhi na kusindikizwa na Gwaride kuelekea Ikulu majira ya 12:00 mchana kabla ya saa 8:00 kupelekwa katika Bunge la nchi hiyo na watu kutoa heshima za mwisho majira ya saa 12 jioni.
Mnamos siku ya Ijumaa, msafara utaelekea Kisumu na Bondo kwa ajili ya watu kutoa heshima zao katika ibada ya kitaifa itayofanyika katika Uwanja wa Nyayo, ikihudhuriwa na viongozi kutoka ndani na nje ya nchi kabla ya kupelekwa kanisani katika Ibada ya kuuaga mwili wa Waziri huyo wa zamani wa taifa hilo Jumamosi, katika Uwanja wa Moi, Kisumu, na wananchi wataruhusiwa kuuaga kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi 9:00 alasiri na mazishi kufanyika siku ya Jumapili.