Biashara ya dhahabu feki yaibuka

Jumatatu , 26th Apr , 2021

Serikali imewaonya watu wanaojihusisha na utapeli wa kuuza dhahabu feki kwa kutumia vyuma vilivyozungushiwa vumbi la dhahabu kisha kuwauzia watu, kuwa wahusika wote wa biashara hiyo haramu watatiwa nguvuni.

Kushoto ni Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Joseph Kumburu, Kulia ni madini ya dhahabu (Picha kutoka mtandaoni)

Hayo yameelezwa na Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Joseph Kumburu, katika mkutano wa kutoa elimu ya biashara ya madini, uliofanyika kwenye migodi ya Imalamate Wilaya ya Busega, ulioshirikisha vyombo vya kiusalama, wamiliki wa migodi na maduara, ambapo  Mkurugenzi wa Mgodi wa EMJ uliopo Dutwa, Bariadi, akashauri mgao wa mawe mgodini hapo ufanyike kila siku kuanzia leo 26/04/2021.

"Kuna watu wamenunua dhahabu, juzi tumekamata watu na dhahabu feki, wanakuja hapa na wanaleta chuma wanazungushia dhahabu, baada ya kupata hiyo taarifa tukawaweka watu kuchunguza hakuna aliyekuwa anajua, baadae tukaweka mtego tumepata na vigoroli vile, haya mambo tunawasidia nyinyi mnaibiwa, na nyinyi mkiona toeni taarifa kwetu  au polisi" amesema Mhandisi Kumburu

Aidha kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Busega Tano Mwera amesema kuwa ule mtindo wa wachimbaji kukusanya viroba ndio mgao ufanyike haupo tena badala yake mgao utafanyika hata kama mtu mmoja au wawili wana viroba.