Jumanne , 18th Nov , 2025

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuunga mkono azimio lililoandaliwa na Marekani linalounga mkono mpango wa vipengele 20 wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Gaza.

Kilichojumuishwa katika mpango huo ni kuanzishwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Udhibiti (ISF), ambacho, Marekani inasema, nchi nyingi ambazo hazijatajwa majina zimejitolea kuchangia.

Azimio hilo liliungwa mkono na nchi 13, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa na Somalia, bila hata moja kupiga kura kupinga pendekezo hilo.

Urusi na China zilijizuia. Kulipitisha lilikuwa "hatua muhimu katika kuimarisha usitishaji mapigano," msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema. Hamas imekataa azimio hilo, ikisema halikukidhi haki na matakwa ya Wapalestina.

Ikiandika kwenye Telegram baada ya azimio hilo kupitishwa, Hamas ilisema mpango huo, "unaweka utaratibu wa ulinzi wa kimataifa katika Ukanda wa Gaza, ambao watu wetu na makundi yao wanaukataa".