Washukiwa wawili wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa vito vya thamani ya Euro 88M sawa na zaidi ya shilingi bilioni 240 kutoka kwenye jumba la makumbusho la Louvre mjini Paris wamekamatwa.
Wanaume hao wawili, wenye umri wa kati ya miaka 30 kutoka kitongoji cha Seine-Saint-Denis kaskazini mwa Paris, waliwekwa chini ya ulinzi jana Jumamosi jioni kama sehemu ya uchunguzi ulioongozwa na kitengo cha uhalifu uliopangwa cha Paris.
Kulingana na ofisi ya mwendesha mashtaka wa Paris mmoja wa washukiwa hao alinaswa Jumamosi Oktoba 25, mwendo wa saa 10 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle alipokuwa anakaribia kupanda ndege nje ya nchi, inayoripotiwa kuelekea Algeria. Wa pili alikamatwa baadaye jioni hiyo hiyo huko Seine-Saint-Denis, gazeti la Ufaransa Le Parisien liliripoti.
Kukamatwa kwa watu hao kunakuja wiki moja baada ya genge la wanaume wanne kufanya moja ya wizi wa kutisha zaidi katika historia ya Ufaransa. Wakijifanya kama wafanyakazi wa ujenzi na wakiendesha lori lililoibiwa la kuondoa fanicha lililowekwa lifti, walifika kwenye makumbusho ya Louvre mwendo wa saa 9:30 asubuhi na kutumia mashine hiyo kufikia Jumba la sanaa la Apollo ambapo ni nyumbani kwa baadhi ya sanaa za kifalme zinazothaminiwa zaidi za Ufaransa.
Polisi wa Ufaransa wamesema wezi hao walitumia lifti iliyopandishwa ndani ya gari kuingia kabla ya kuwatishia walinzi wa jumba la makumbusho, wakaiba vito na kutoroka kwa pikipiki, wakikamilisha wizi huo ndani ya dakika nne.
Vyombo vya habari vya Ufaransa vilielezea tukio hilo kama "aibu ya kitaifa," na kusababisha uchunguzi mpya wa itifaki za usalama za Louvre.
Polisi bado hawajathibitisha kama vito vilivyoibiwa ambavyo ni pamoja na vipande vilivyokuwa vya Napoleon III na Empress Eugénie vimepatikana. Mwendesha mashtaka wa Paris Laure Beccuau amethibitisha leo Jumapili kwamba mmoja wa watu hao alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle kaskazini mwa Paris alipokuwa akikaribia kuondoka nchini. Hakusema katika taarifa yake ni wanaume wangapi walikamatwa au kutoa maelezo zaidi. Uchunguzi unaendelea. #EastAfricaTV

