
Katibu Mwenezi wa ACT- wazalendo, Ado Shaibu
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es salaam, Katibu Mwenezi wa chama hicho, Ado Shaibu amesema kuwa mfumo wa kutunza samaki wa nchi umekuwa wa kikoloni na hauwezi kuwa na tija kwa taifa.
"Tumefanya utafiti kwa miaka miwili juu ya oparesheni za serikali katika kupambana na uvuvi haramu, tumegundua matatizo gani ambayo yanatakiwa kushughulikiwa ili mambo yawe bora zaidi," amesema.
"Vipo vitendo vya kinyama vinavyojumuisha matukio ya kuua, kuwatesa, kuwaweka kizuizini, kuwatweza na kuwaumiza wavuvi na wafanyabiashara imekuwa kawaida, na sisi tumekusanya na tutaendelea kukusanya matukio haya," ameongeza.
Pia Katibu huyo Mwenezi wa ACT amesema kuwa waliongea na wavuvi katika bahari ya Hindi mwezi Julai mwaka uliopita, ambapo walielezwa kuwa mwenzao aliyejulikana kwa jina la Masoud Juma Masoud aliuwawa na wanodaiwa kuwa ni askari, siku ambayo ilikuwa ni 'Siku ya Bahari Duniani' na kudai kuwa jambo hilo licha ya kufikishwa katika Kamati ya Bunge halikushughulikiwa.
ACT imesisitiza kuwa haitokaa kimya katika masuala ya kutetea haki za wananchi na kuitaka serikali kuendesha uchunguzi juu ya vifo vya wavuvi waliopotea katika ziwa Manyara, Geita pamoja na Masoud Juma Masoud aliyepotea katika bahari ya Hindi.