Jumanne , 14th Jun , 2022

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amependekeza kufutwa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili kuwapunguzia gharama.

Akisoma bajeti ya mwaka 2022/2023 Waziri Nchemba amesema kwa sasa wanafunzi wa kidato cha tano ni takribani 90,825 na kidato cha sita ni 56,880 na mahitaji ya fedha ni Sh10 3 bilioni.
Aidha kuhusu vyuo vya kati amesema serikali  itajipanga kuangalia namna ya kusaidia vyuohivyo kadiri hali ya uchumi itakavyotengemaa.

Amebainisha kuwa Kwa hatua hiyo, elimu bila ada ni kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha sita,”
Katika hatua nyingine amesema kuwa Hadi kufikia Aprili 2022 deni la serikali lilikuwa trilioni 69.44 sawa na ongezeko la asilimia 14.4 ikilinganishwa na trilioni 60.72 April 2021, kati ya hizo deni la ndani ni trilioni 22.37 sawa na asilimia 32.2 na deni la nje ni trilioni 47.07 sawa na asilima 67.8

Katika mwaka 2022/23, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 41.48 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo ambapo  Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 26.48 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 63.8 ya bajeti yote, ikijumuisha shilingi trilioni 11.31 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu na shilingi trilioni 9.83 kwa ajili ya mishahara ikiwemo nyongeza ya mshahara, upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya. Aidha, shilingi trilioni 5.34 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ikijumuisha shilingi bilioni 200.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi na wazabuni.

"Sura ya Bajeti kwa mwaka 2022/23 inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 41.48 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 28.02, sawa na asilimia 67.5 ya bajeti yote" 

"Kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 23.65 na mapato yasiyo ya kodi (Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 4.37"  ameeleza Dkt.Mwigulu Nchemba

Aidha Waziri Nchemba amesema Bajeti hiyo inalenga kumsaidia Mtanzania hasa kumuepusha na mfumuko wa bei unaosababishwa na majanga yanayoendelea duniani huku ikilenga pia kupunguza baadhi ya matumizi ya serikali 

"Tumezidi mno kupenda ubosi, magari makubwa kwa kila mtu serikalini, matumizi ya starehe katika nchi hiyo hiyo kuna watu wanapata shida kupata mlo mmoja, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Fedha na Mipango ifanye kazi kwenye jambo hili na iweze kuleta mapendekezo ya namna fedha hizi ziweze kutumika kwenye matumizi ya msingi tu" 

"Napendekeza yeyote aliyeko kwenye nafasi ya kuteuliwa akitolewa lakini akabaki kwenye utumishi wa umma arejee pia kwenye mshahara aliokuwa analipwa kabla ya kuteuliwa, hii itawapunguzia mzigo watanzania kulipa watu walioko bench"