Jumanne , 23rd Dec , 2025

Mwanafunzi huyo anadaiwa kutoweka nyumbani kwao kijiji cha Kivulini baada ya kubainika kuwa na ujauzito.

Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Kileo iliyopo kata ya Kileo wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro amekatisha masomo baada ya kudaiwa kupewa ujauzito na kijana mmoja aliyetajwa kwa jina la Fadhili mkazi kijiji cha kivulini kata ya Kileo

Mwanafunzi huyo anadaiwa kutoweka nyumbani kwao kijiji cha Kivulini baada ya kubainika kuwa na ujauzito.

Akizungumza EATV mama mzazi wa Mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mwavita Ramadhani Mmbaga alidai aligundua mwanaye anaujauzito mara baada ya kuona mabadiliko ya kiafya na alipombana alikiri kuwa na ujauzito na kumtaka aliyempa ujauzito .

Mwavita alidai kuwa wamesharipoti taarifa ya mtoto wake kupewa ujauzito kituo cha polisi Mwanga dawati la jinsia.

Amesema aliongozana polisi pamoja mwanafunzi huyo kwenda kumpima ambapo vipimo vilionyesha kuwa na ujauzito wa miezi minne.

Taarifa hiyo aliripoti Novemba 20,2025 na kupewa RB...MWG/IR/1554/2025,ambapo mpaka sasa anadai hakuna hatua zilichukuliwa na mwanafunzi huyo hajulikani alipo.

"Binti yangu alitoroka nyumbani usiku na nikatoa taarifa polisi wakaenda mpaka nyumba kwa kijana huyo usiku wamanane na wakawakuta wote lakini wanadai walimchukua mtuhumiwa wakamwacha binti huyo,"amesema Mwavita mama mzazi wa mwanafunzi huyo.

"Hata huyo kijana bado anaonekana mitaani lakini polisi Mwanga wanadai wamemkamata ,"amesema.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro SACP Simon Maigwa alipotafutwa kwa njia ya simu hukusu taarifa hiyo alidai kuwa hana taarifa hiyo na kwamba ataifuatilia.