Jumanne , 16th Sep , 2025

Imeelezwa kuwa watoto hao walianza kuogelea kabla ya kushindwa kuyamudu maji na Lilian Mandali kujitosa ili kuwaokoa kabla ya kuzama pia na kufariki dunia.

Mfanyakazi wa benki ya NMB amefariki dunia baada ya kuzama katika maporomoko ya maji yaliyopo Hifadhi ya Mpanga Kipengere, mkoani Njombe wakati akijaribu kuwaokoa watoto wawili ambao hata hivyo walipoteza maishja pia.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amesema mkasa huo umetokea Septemba 14, 2025 majira ya saa nane na nusu mchana, wakati wa sherehe ya pamoja (get together) ya wafanyakazi wa NMB kutoka matawi ya Makambako, Wanging’ombe na Makete.

Waliofariki ni Michelle Mwasongwe (5) na Jannel Mwasongwe (4), ambao ni watoto wa Bertha Nicodem ambaye ni mfanyakazi wa NMB tawi la Makambako, pamoja na Lilian Mandali (31).

Imeelezwa kuwa watoto hao walianza kuogelea kabla ya kushindwa kuyamudu maji na Lilian Mandali kujitosa ili kuwaokoa kabla ya kuzama pia na kufariki dunia.

Miili ya marehemu hao imeopolewa na kuhifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Mbuyuni wilayani Mbarali.