Afisa aliyekamata bangi milimani, ateuliwa na Rais

Jumatatu , 6th Jul , 2020

Rais Magufuli amempandisha cheo aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, Bw. James Kaji na kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo.

Rais Magufuli akimuapisha Kamishna James Kaji

Amefanya uteuzi huo leo, Ikulu Chamwino Jijini Dodoma alipokuwa akihutubia baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Wakuu wa Wilaya aliowateua hivi karibuni, ambapo amemuapisha afisa huyo kuanza kuitumikia kazi yake.

Rais Magufuli amesema amemteua Bw. James Kaji kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri anayoifanya, baada ya kutembelea Wilayani Meru na kukamata magunia ya bangi na kuyateketeza.

"Jana nilikuona wa madawa unapita kwenye milima kule, unapita kwenye mji unakuta magunia ya bangi, IGP nataka Mkuu wa Polisi wa Meru aondolewe na Afisa Usalama wa wilaya hiyo naye aondolewe. Wewe Kamishna wa Madawa ya Kulevya leo mimi nakuthibitisha umefanya kazi nzuri. Nataka mambo yaonekane", amesema Rais Magfuli.

"Madawa ya Kulevya mpaka mtu atoke Dar es Salaam ndiyo akayaone wakati hapo kuna Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, OCD?. Kila mmoja afanye majukumu yake, najisikia raha kufanya kazi na watu wachapakazi", ameongeza.