Jumanne , 18th Oct , 2016

Watu 10 wamefariki dunia papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la abiria mali ya kampuni ya Barcelona iliyotokea eneo la Mpeja, Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi jana Asubuhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Renatha Mzinga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Renatha Mzinga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubanisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva uliosababisha kushindwa kulimudu basi hilo baada ya kupasuka tairi.

Kamanda Mzinga amesema jeshi hilo linamshikilia kondakta wa basi hilo ambaye jina lake halijajulikana kutokana na kujeruhiwa vibaya na kushindwa kuongea huku wakimtafuta dereva wa basi hilo ambaye alitoweka baada ya ajali hiyo.

Aidha Kamanda Mzinga ametumia nafasi hiyo kuwataka madereva wa magari ya abiria na mizigo kuzingatia sheria kanuni na taratibu za matumizi ya barabara ili kuepuka kupoteza maisha ya watu wasio na hatia na mali zao.

Hadi tunaenda mitamboni Kamanda Mzinga amesema kuwa majina ya watu waliofariki dunia bado hayajafahamika huku majeruhi 40 kati ya 44 wakikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Kinyonga katika mji Mkongwe wa kivinje.