Jumanne , 29th Jul , 2025

Kati ya wanajeshi 19,000 waliojeruhiwa tangu mauaji ya halaiki yalipoanza, takriban 10,000 wanakabiliwa na dalili za kisaikolojia na wanapata matibabu kupitia idara ya urekebishaji ya Wizara ya Ulinzi.

Visa vya wanajeshi wa Israel kujiua  vimefikia  54 tangu mauaji ya halaiki huko Gaza yalipoanza Oktoba 2023, hii ni kulingana na shirika la utangazaji la umma la Israeli, KAN.

Tangu mwanzoni mwa mwaka 2025, wanajeshi kumi na sita wa Israeli wamejiua. Takwimu za hivi karibuni zinajumuisha wanajeshi wanane wa kazi, wanajeshi saba wa akiba, na mwanajeshi mmoja wa taaluma. Mnamo mwaka 2024, wanajeshi 21 walifariki kwa kujiua, na mwaka 2023 idadi hiyo ilikuwa 17.

Shirika hilo la KAN limeonyesha ongezeko kubwa la viwango vya kujiua miongoni mwa wanajeshi wa akiba, ambao wamekuwa wakitumwa kwa wingi Gaza kwa ajili ya uvamizi wa ardhini wa Israeli. Aidha, karibu wanajeshi 3,770 wamegunduliwa kuwa na ugonjwa wa msongo wa mawazo baada ya tukio (PTSD), kulingana na ripoti ya KAN.

Kati ya wanajeshi 19,000 waliojeruhiwa tangu mauaji ya halaiki yalipoanza, takriban 10,000 wanakabiliwa na dalili za kisaikolojia na wanapata matibabu kupitia idara ya urekebishaji ya Wizara ya Ulinzi.

Jeshi la Israeli limekuwa likiandaa warsha za kukuza uimara wa kisaikolojia na linawapeleka wanajeshi waliopigana kwa wanasaikolojia wa kijeshi kwa lengo la kukabiliana na kile maafisa wanachokiita hali ya kutia wasiwasi.