"Akijichanganya tunachapa"- Msukuma

Jumanne , 13th Feb , 2018

Mbunge na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma amefunguka na kudai upinzani wa kweli upo ndani ya CCM na wala sio kata vyama vingine kwa maana Waziri yeyote akifanya ndio sivyo wana uwezo wa kumuadabisha.

Msukuma ametoa kauli hiyo mbele ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam eneo la Kigogo wakati akimuombea ridhaa mgombea wao Maulid Mtulia ili aweze kupigiwa kura za ndio kwa wingi mnamo Februari 17 mwaka 2018 ambapo uchaguzi wa marudio utafanyika katika Jimbo la Kinondoni pamoja na Siha.

"Leo kuna machinga yeyote ambaye ananyanyaswa Dar es Salaam si hakuna na imetolewa amri sasa waliokamatwa na bodaboda na Polisi waachiwe lakini hawa jamaa wanasema CCM ni mbaya. Wanataka Magufuli akalale na wake zao ndio waone CCM ni nzuri",amesema Msukuma.

Pamoja na hayo, Msukuma ameendelea kwa kusema "upinzani wa kweli upo CCM ndio maana mnaona sisi Waziri yeyote akijichanganya tunachapa na tunamwambia Rais kuwa huyu hafai anatoka. Mimi nimefanya kazi na Lowassa mwaka 2015 nilikuwa nazunguka nae kwenye 'helkopta' yake".

Kwa upande mwingine, Msukuma aliwataka wananchi hao endapo Mhe. Freeman Mbowe atakanyaga eneo hilo basi wamuulize zile pesa alizouza chama cha CHADEMA amezipeleka wapi kwa madai ameshindwa hata kujenga ofisi ya chama katika eneo hilo la Kigogo.