Jumatano , 15th Apr , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kufuatia vifo vya watu 18 vilivyotokea wilayani Mkuranga mkoani Pwani, kutokana na ajali ya gari iliyohusisha gari ndogo na Lori la mizigo Alfajiri ya leo Aprili 15, 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, na kusema kuwa ajali hiyo imehusisha gari ndogo ya abiria aina ya Coaster iliyokuwa ikitoka kijiji cha Magawa wilayani humo kuelekea Jijini Dar es Salaam na Lori lilikuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Kusini.

"Nawaombea familia za marehemu wote, ndugu, jamaa na marafiki kuwa na moyo wa uvumilivu na ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, kuwapoteza Watanzania wenzetu kwa idadi kubwa namna hii inaumiza sana" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amewataka madereva wa vyombo vya moto, wanaotumia barabara kuzingatia sheria za barabarani ili kuepusha ajali zinazogharimu maisha ya watu wengi.