Jumatano , 15th Jul , 2020

Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu kupitia CHADEMA, Gimbi Masaba, ameshindwa katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya chama hicho baada ya kupata kura 83 dhidi ya 161 alizopata mshindani wake, Machumu Maximilian.

CHADEMA

Gimbi aliyehudumu katika Bunge kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015 hadi mwaka huu 2020, ameshindwa katika kinyang'anyiro cha kuomba ridhaa kugombea Ubunge Jimbo la Itilima, mkoani Simiyu.

Uchaguzi huo wa kura za maoni ulimalizika Saa 2 kasorobo usiku wa Julai 14, ambao uliofanyika kwa njia ya wazi eneo la Lagangabilili, wilayani Itilima chini ya Msimamizi wa Uchaguzi  Joseph Ndatala.

Baada ya uchaguzi huo, Gimbi Masaba amekubaliana na matokeo hayo huku Maximilian aliyetangazwa mshindi akiwashukuru wajumbe wote waliompigia kura.

Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, matokeo yote ya uchaguzi ndani ya chama hicho huidhinishwa na Kamati Kuu ya Taifa kabla ya kuanza rasmi Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.