Aliyepofuka macho kisa mkopo apewa neno

Ijumaa , 15th Mar , 2019

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu imesema ipo tayari kutoa mkopo kwa mwanafunzi Nelson Mubezi ambaye anatajwa alipata matatizo ya upofu baada ya kukosa mkopo.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mawasiliano wa bodi ya mikopo, Veneranda Malima wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa BreakFast cha East Africa Radio.

Veneranda amesema kuwa, "tuliamuangalia mwanafunzi (Nelson Mubezi) aliyepofuka kwenye kumbukumbu zetu hakuwahi kuwa mteja wetu, japo tulimuona kwenye orodha ya wanafunzi waliodahiliwa lakini hakuomba mkopo, huwezi kupata mkopo kama hukuomba".

"Baada ya kuiona taarifa ya matatizo yaliyompata tukasema kama anasifa basi ataomba na atapangiwa mkopo pia tukamkaribisha kuja kueleza matatizo tutayasikiliza na tutayafanyia kazi", ameongeza Malima.

Hivi karibuni kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini viliripoti taarifa juu ya tukio lililomkuta kijana huyo ambaye amepata maradhi ya upofu baada ya kupatwa na msongo wa mawazo.