Jumapili , 25th Jun , 2023

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amesema kwamba migogoro ya ardhi iliyopo Dodoma kwa sasa haijashuka tu kutoka mbinguni bali kuna chanzo cha migogoro na mtu ambaye anaisababisha yupo hivyo inabidi kumtambua.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo

Kauli hiyo ameitoa hii leo Juni 25, 2023, jijini Dodoma, wakati akihitimisha ziara yake mkoani humo iliyokuwa na lengo la kuimarisha chama, kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali pamoja na kuangalia uhai wa chama hicho.

"Hakuna mgogoro wa ardhi unaotoka mbinguni ukashuka na kuwakuta watu wakiwa salama na kuwa mgogoro, mgogoro wowote wa ardhi ujue yupo mtu anayeutengeneza, lazima kipo chanzo husika, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi hatuwezi kupaacha kuwa sehemu ya migogoro," amesema Chongolo

Aidha Chongolo ameongeza kuwa, "Lazima tuweke mipango ya kutatua migogoro Dodoma, na sisi tutaingia katikati kufuatilia hatua kwa hatua kuona ni namna gani tunaenda kumaliza migogoro hii, tujue ni nani aliyeisababisha na yuko wapi sasa, na waliopata madhara hayo wanafanyiwa nini ili kuondokana na madhira hayo".