Jumatatu , 15th Sep , 2025

Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba Baraza la Haki za Kibinadamu litakutana kwa dharura kesho Jumanne Septemba 16, kujadili mashambulizi ya Israel nchini Qatar ambayo yaliwalenga viongozi wa Hamas wa Palestina huko Doha wiki iliyopita 

Mjadala huu wa dharura unaitishwa kujibu maombi mawili rasmi yaliyowasilishwa siku ya Jumatano ya wiki iliyopita na Pakistan, kwa niaba ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), na Kuwait, kwa niaba ya Baraza la Ushirikiano la Nchi za Kiarabu za Ghuba,

Baraza hilo litajadili uchokozi wa kijeshi wa hivi majuzi uliofanywa na Israel dhidi ya Qatar mnamo 9 Septemba, 
Huu ni mjadala wa kumi wa dharura tangu kuundwa kwa Baraza la Haki za Kibinadamu mwaka 2006.

Shambulio la Israel, ambalo liliwalenga viongozi wa Hamas, lilitekelezwa dhidi ya makazi ya watu huko Doha, mji mkuu wa nchi hiyo inayopatanisha mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Mashambulio hayo ya Israel yalisababisha vifo vya wanachama watano wa vuguvugu la Palestina na askari wa kikosi cha usalama cha Qatar, lakini vuguvugu hilo la Kiislamu lilisema maafisa waliolengwa walinusurika.

Mashambulizi hayo yamishtumiwa na nchi nyingi, hasa nchi  tajiri za Ghuba, washirika wa Marekani.