Jumanne , 11th Oct , 2016

Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Bi. Ashatu Kijaji imesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini TADB ni kiungo muhimu baina ya serikali na wakulima katika kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo.

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Bi. Ashatu Kijaji

Amesema umuhimu huo unaongezeka hasa kipindi hiki ambapo sekta hiyo ndiyo tegemeo kuu la utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo, Naibu Waziri Kijaji amesema uwepo wa benki ya kilimo inayojiendesha kwa mtazamo wa kisera ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia sabini ya watanzania wameajiriwa kwenye kilimo huku sekta hiyo ikichangia zaidi ya asilimia 28 ya pato la taifa.

Uhaba wa mtaji pamoja na mipango ya kujitanua kibiashara ni moja ya changamoto zinazoikabili benki hiyo katika juhudi zake za kufikia idadi kubwa ya Watanzania ambapo Mkurugenzi Mtendaji Thomas Samkyi amesema suala la kudhibiti riba kuwa ndogo na gharama kubwa za uendeshaji wa mabenki ni moja ya eneo linalowapa changamoto kubwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Bi. Rosebud Violet Kurwijila amesema kutokana na uchanga wa taasisi yake, changamoto inayowakabili ni pamoja na kuandaa mpango biashara utakaowawezesha kufikia idadi kubwa ya Watanzania.