Ijumaa , 5th Sep , 2025

Msemaji wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden amesema kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Marekani amefanyiwa upasuaji wa saratani ya ngozi

Haijulikani ni lini alifanyiwa upasuaji huo, lakini video ya mwishoni mwa Agosti ilionyesha akitoka kanisani huko Delaware akiwa na kovu kubwa jipya kichwani.

Msemaji huyo ameviambia vyombo vya habari kuwa anaendelea kupata afueni.

Upasuaji wa Biden ulihusisha kuondoa safu ya tishu, kuichunguza chini ya darubini ili kuona ikiwa kuna chembechembe za saratani zilizosalia, na kurudia ikiwa kutakuwa na lazima ya kufanya hivyo.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 82 alikuwa na ‘basal cell carcinoma’, mojawapo ya aina mbili za saratani ya ngozi, iliyoondolewa kifuani mwake mwaka wa 2023.

Daktari wake alisema wakati huo kwamba seli zote za saratani zilikuwa zimeondolewa.

Mwaka huo huo, mke wa Bw Biden, Jill, aliondolewa saratani mbili za ‘basal cell carcinomas’ karibu na jicho lake na kifuani mwake.

Rais huyo wa zamani pia alifichua mwezi wa Mei mwaka huu kwamba alikuwa na saratani ya tezi dume ambayo iko hatua ya nne - huku ugonjwa huo ukisambaa hadi kwenye mifupa.