Jumamosi , 23rd Mar , 2024

Bilionea na mfanyabiashara Mustafa Rajabali Jaffer, maarufu kwa jina Bilionea Sabodo amefariki dunia leo Machi 23, 2024 akiwa nyumbani kwake Masaki ambapo kwa mujibu wa mtoto wake taratibu za mazishi zinaendelea na maziko yatafanyika makaburi ya mtaa wa Bibi Titi Mohamedi.

Bilionea Mustafa Rajabali Jaffer (Sabodo)

Enzi za uhai wake Sabodo alikuwa akisaidia maendeleo ya huduma za jamii na uimarishaji wa Demokrasia ambapo aliwahi kuchangia fedha kwa nyakati tofauti kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwaka 2003 Sabodo alitoa udhamini wa uchezeshaji wa bahati nasibu ya mfuko wa Mwalimu J.K Nyerere wenye thamani ya Sh 100 milioni.

Wazo la kuanzishwa kwa mfuko huo wa Mwalimu Nyerere lilikuwa la Sabodo, pia alichangia Sh 1.3 bilioni katika kuufanikisha.

Pia Sabodo amechangia miradi mbalimbali ikiwemo kutoa kiasi cha Sh 5 bilioni kwa ajili ya kuchangia chuo cha ualimu cha elimu ya juu cha Mtwara, alichangia Sh 965 milioni kwa ajili ya upanuzi wa majengo ya hospitali ya Shree Hindu Mandal, mradi wa Khoja Shia-aheri Sh 1.6 bilioni.