Jumapili , 24th Jul , 2022

Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka waendesha bodaboda na bajaji nchini kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika zoezi la sensa huku akiwataka kulinda hadhi ya kazi zao kwa kuepuka kashifa ya vitendo vya uporaji na ujambazi kwani sekta yao ni muhimu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,

Rais Samia aliyasema hayo leo Jijini Dodoma kwa njia ya simu katika kongamano la kuimarisha ushiriki wa waendesha bodaboda na bajaji katika sensa ya watu na makazi ambapo amesema kuwa yuko tayari kutatua changamoto za madereva bodaboda ili walinde heshima yao.

"Ninyi ni watu muhimu sana katika Taifa letu, kuna baadhi yenu wanawaharibia sifa niwasihi msikubali kuharibiwa sifa na baadhi yenu ambao wanautumia usafiri huo kwa kupora, kukaba na kutumika katika ujambazi," amesema Rais Samia 

Aidha Rais Samia akaongeza, "Elezeni changamoto zenu zote mkuu wa mkoa ataniletea na mimi nimeahidi kuzitekeleza changamoto zenu ikiwa ninyi ni sekta muhimu kwa wananchi wa hali ya chini kutokana na huduma mnayoitoa,".