Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin akikabidhi mfano wa hundi kwa ajili ya kusaidia maafa ya waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera Ikulu jijini Dar es salaam kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin amekabidhi hundi zenye jumla ya USD 250
Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohra Duniani Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin amekabidhi mchango huo kwa Rais Magufuli, walipokutana na kufanya Mazungumzo leo tarehe 13 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kati ya fedha hizo Dola za Marekani laki moja (Usd. 100,000) zimetolewa na Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin mwenyewe, Dola za Marekani laki moja (Usd. 100,000) zimetolewa na Viongozi wengine wa Madhehebu ya Bohra na Dola za Marekani Elfu Hamsini (Usd. 50,000) zimetolewa na wana Jumuiya ya Bohra wa Tanzania.
Pamoja na kutoa mchango huo, Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa Jumuiya hiyo ambayo inamiliki hospitali kubwa zilizopo maeneo mbalimbali duniani ikiwemo India, itajenga hospitali hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu.
Pia Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin ameahidi kuwa Jumuiya ya Bohra itatoa udhamini wa masomo ya udaktari kwa vijana wa Tanzania na pia itadhamini matibabu kwa wagonjwa 20 watakaopelekwa nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kwa Upande wake Rais Magufuli, amemshukuru Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin na Jumuiya nzima ya Dawoodi Bohra kwa mchango walioutoa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera na pia kwa kufanyia mkutano wao wa mwaka hapa nchini uliowaleta wageni takribani 31,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Jumuiya ya Madhehebu ya Dawoodi Bohra Duniani imeadhimisha mwaka mpya wa Kiislam na kumbukumbu ya kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W) aitwaye Imamu Hussein ambapo maadhimisho yake ya kidunia yaliyoambatana na tamasha la zaidi ya wiki mbili yamefanyika hapa nchini kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2016 hadi tarehe 11 Oktoba, 2016.