Ijumaa , 15th Aug , 2014

Wanafunzi kumi kutoka nchini Tanzania wameteuliwa kwenda nchini Uingereza kusomea digrii ya pili katika fani za mafuta na gesi, mafunzo yatakayochukua kipindi cha mwaka mmoja.

Fursa ya wanafunzi hao kwenda kusomea fani hizo imetolewa kwa udhamini wa Kituo cha ushirikiano wa masuala ya kielimu, utamaduni na kijamii cha serikali ya Uingereza nchini Tanzania cha British Council, kwa kushirikiana na kampuni ya gesi kutoka nchini Uingereza na ambayo inafanya shughuli zake hapa nchini ifahamikayo kama ya British Gas.

Mkurugenzi wa Miradi ya Elimu na Sanaa wa British Council, Bi. Nesia Mahenge amezungumzia umuhimu wa wanafunzi hao kwenda kusoma nje ya nchi na kwamba mara watakaporudi watakuwa na mchango mkubwa katika uchumi na maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, mmoja wa wanafunzi hao Epiphania Kimaro amesema mchakato wa kupata udhamini huo ulikuwa wa wazi tofauti na michakato mingine ambayo imekuwa na tuhuma za upendeleo ambapo ameahidi kutumia elimu atakayoipata kwa manufaa ya ukuaji wa uchumi.