
Akielezea masikitiko yake katika kipindi cha Hot Mix cha EATV Mtatiro amesema kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) imewekwa wabunge wageni kutoka upinzani na kamati hiyo inatakiwa kuongozwa na mbunge kutoka upinzani hivyo lengo la kuisimamia serikali halijapewa kipaumbele.
''Rais Magufuli alipolihutubia bunge aliomba kupewa ushirikiano wa hali ya juu kuchagua wabunge wapya wa kusimamia hesabu za serikali ni kuwapa wabunge hao mzigo mzito, kamati hii ilikuwa ikiongozwa na Zitto na serikali iliona uwezo wake ndiyo maana wametafuta watu ambao hawana uzoefu jambo ambalo sii zuri'' Amesisitiza Mtatiro.
Mtatiro ameongeza kuwa ''Spika Ndugai hakuhitaji elimu ya chuo kikuu katika kufanya uteuzi wa kamati hizi na sidhani kama kuchagua kamati dhaifu kama hizi kunamaanisha dhana ya Rais Magufuli ya hapa kazi tuu''.
Katika hatua nyingine Mtatiro amepongeza ushindi wa mbunge wa Mwibara wa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati ya hesabu za mitaa LAAC kwa kuwa ni mtu ambaye ana uwezo mkubwa na msimamo katika kusimamia mambo yenye maslahi ya taifa, huku akikosoa tena aina ya wabunge kutoka upinzani waliowekwa kwenye kamati hiyo.
Kuhusu kamati ya Nishati na Madini kuongozwa na mbunge wa viti maalum CCM Martha Mlata, Mtatiro amesema kuwa Martha hatoshi katika nafasi hiyo, na vema CCM ikaweka wabunge wengine wenye uwezo mkubwa waliomo katika kamati hiyo.
Kuhusu Tume ya uchaguzi Zanzibar kutangaza tarehe ya uchaguzi Mtatiro amesema kilichofanyika Zanzibar ni makusudi matupu na kama CUF haitashiriki katika uchaguzi huo ni wazi kuwa kutakuwa na sintofahamu kisiwani humo.
Amesema tatizo la nchi nyingi za kiafrika ni kuwa na katiba mbovu ambazo hazitoi mwanya wa kupinga matokeo, kwa maana hiyo CUF kaa sasa haina cha kufanya maana hakuna hata fursa yoyote ya kikatiba au kisheria kuzuia uchaguzi huo.
"Kitu ninachoweza kusema ni kwamba kutakuwa na vurugu sana, kabla ya uchaguzi au baada ya uchaguzi"