
Shirika lisilo la kiserikali la CCBRT na hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wamezindua ushirikiano wenye lengo la kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika jiji la Dar es salaam na kwa kuanzia CCBRT imekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 50 ili kusaidia vifaa vya watoto wadogo hospitalini hapo.
Akiongea wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Mama na Mtoto CCBRT Suzan Boon amesema kuwa katika kuendelea kuimarisha huduma za mama na mtoto wameandaa kamati maalum itakayoshughulikia uimarishaji wa mifumo ya rufaa ili kupunguza vifo vya wajawazito na vichanga vinavyotokea hospitalini hapo.
Aidha, CCBRT imesema inaendelea na ujenzi wa hospitali mpya ya mama na mtoto inayotarajiwa kukamilika mapema mwaka 2018 hospitali ambayo itakuwa ni teule ya ya uzazi ya rufaa na itapokea rufaa zote za wajawazito wenye matatizo makubwa ya uzazi.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto wadogo katika hospitali ya Muhimbili Edina Majaliwa amesema kuwa vifaa vya kuwasaidia wazazi na watoto wachanga vinavyotolewa na CCBRT vimeonekana kusaidia kupunguza idadi ya vifo vya watoto wadogo vinavyotokea hospitalini hapo.