Jumanne , 4th Aug , 2015

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa wanaozania kuwa CCM ni chama cha mchezo watakiona cha mtemakuni katika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu.

Dk. Kikwete ambaye pia ni rais wa Jamuhri ya Muungano wa Tanzania, amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa katika uchaguzi huo CCM watafunga magoli huku upinzani wakiishia kutazama tu.

Dk. Kikwete ambaye alikuwa akimkaribisha mgombea wa CCM Dk. John Pombe Magufuli mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania urasi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, amesema CCM haiwezi kumdharau adui yoyote kwa kuwa hii ni vita.

Akiongea katika mkutano huo Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana amesema kuwa katika uchaguzi huu CCM kinapambana na makapi yake hivyo hakitapata tabu kushinda kauli ambayo inamlenga mgombe wa Chadema Mhe. Edward Lowassa ambaye amejiondoa CCM.