Alhamisi , 31st Jul , 2025

Wakili Flory amebainisha kuwa jitihada zilizofanyika zimeifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara kwa nchi za ushoroba wa kati ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Malawi, Uganda pamoja na Zambia.

Katibu Mtendaji wa Wakala wa uwezeshaji wa usafiri wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA) Wakili Okandju Okonge Flory  amebainisha kuwa mafanikio ya miradi ya Kikanda ya usafiri na usafirishaji nchini yametokana na Uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mtandao wa usafiri na  usafirishaji wa Kikanda.

Wakati wa uzinduzi wa Bandari kavu ya Kwala Mkoani Pwani pamoja na mapokezi ya Mabehewa mapya na yaliyokarabatiwa ya reli ya MGR leo Julai 31, 2025, mbele ya Rais Samia, Wakili Flory amebainisha kuwa  jitihada hizo zimeifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara kwa nchi za ushoroba wa kati ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Malawi, Uganda pamoja na Zambia.

Flory ameeleza kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwasasa imefanikiwa kutoa njia mbadala za usafirishaji zenye ufanisi na gharama nafuu.

Flory ameeleza mchango wa Wakala huo pia katika kufanikisha dhamira ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa wakala huo umesaidia katika afua mbalimbali ikiwemo ukarabati wa mabehewa 20 yenye uwezo wa kubeba tani 800, ikigharimu Shilingi Bilioni 1, lengo likiwa ni kupunguza matumizi ya barabara katika usafirishaji wa mizigo, hatua inayoendana na Malengo ya Dira 2050.

Wakala huo pia umewezesha ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kati ya Tanzania na Burundi na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuwezesha ujenzi wa miundombinu kwenye bandari Kavu ya Kwala pamoja na bandari ya Kalemi na uunganishaji wa reli ya Tanzania na Malawi kupitia TAZARA.